Asante sana Chris. Kila mtu aliyekuja hapa
alisema kuwa anaogopa. Sijui kama na mimi ninaogopa,
lakini hii ni mara yangu ya kwanza kuhutubia hadhara kama hii.
Na sina teknolojia yeyote ya kisasa kwa ajili yenu ili muweze kuiangalia.
Hakuna kielezopicha, kwa hiyo itabidi mnivumilie.
(Kicheko).
Ninachotaka kufanya asubuhi hii ni kuwasimulia hadithi kadhaa
na kuongelea kuhusu Afrika iliyo tofauti.
Tayari asubuhi hii kulikuwa na madokezo kuhusu Afrika
unayoyasikia kila mara: Afrika ya VVU/UKIMWI,
Afrika ya malaria, Afrika ya umaskini, Afrika ya migongano,
na Afrika ya maafa.
Ingawa kuna ukweli kwamba mambo hayo yanatokea,
kuna Afrika ambayo hamuisikii sana.
Na saa nyingine nashangazwa na kujiuliza kwanini.
Hii ni Afrika ambayo inabadilika, ambayo Chris ameidokezea.
Hii ni Afrika yenye fursa.
Hii ni Afrika ambayo watu wanataka kuchukua hatua juu ya
maisha na uwezo wao.
Na hii ndio Afrika ambayo watu wanatafuta kuingia ubia
kufanya hivyo. Na hili haswa ndilo ninalotaka kuzungumzia leo.
Ningependa kuanza kwa kuwaambia
habari kuhusu mabadiliko hayo Afrika.
Mnamo 15 Septemba 2005, Bwana Diepreye Alamieyeseigha,
Gavana wa jimbo moja lenye utajiri wa mafuta huko Nigeria,
alikamatwa na Polisi wa mji wa London alipokuwa matembizini mjini London.
Alikamatwa kwasababu kulikuwa na hamisho la kiasi cha dola za kimarekani milioni 8
ambazo zilienda katika akaunti hewa
ambazo alikuwa akizimiliki yeye pamoja na familia yake.
Kukamatwa kwake kuliwezekana kwasababu kulikuwa na ushirikiano
baina ya Polisi wa mji wa London
na Tume ya Uhalifu wa Kiuchumi na Fedha ya Nigeria --
inayoongozwa na mtu wenye uwezo na ujasiri: Bwana Nuhu Ribadu.
Alamieyeseigha alikamatwa mjini London.
Kutokana na udhaifu, alifanikiwa kutoroka akiwa amevalia kama mwanamke
na kukimbia kutoka London kurudi Nigeria ambako,
kwa mujibu wa katiba, wale walio madarakani
kama magavana, rais – kama ilivyo kwenye nchi nyingi --
wana kinga na hawawezi kushtakiwa. Lakini nini kilitokea:
watu walikasirishwa sana na tabia hii na iliwezekana
kwa sheria za jimbo lake kumvua madaraka.
Leo, Alams – kama tumuitavyo kwa kifupi – yuko jela.
Hii ni hadithi kuhusu ukweli kwamba watu wa Afrika
hawako tayari tena kuvumilia rushwa kutoka kwa viongozi wao.
Hii ni hadithi kuhusu ukweli kwamba watu wanataka rasilimali zao
zidhibitiwe vizuri kwa manufaa yao, na sio kupelekwa sehemu
ambako itawanufaisha mabwanyenye wachache.
Kwa hiyo, unaposikia kuhusu Afrika ya rushwa --
rushwa kila mara – Ninataka mfahamu kuwa watu
na serikali wanajitahidi sana kupambana na tatizo hili
katika baadhi ya nchi, na kwamba mafanikio yanaanza kuonekana.
Inamaana kuwa tatizo limekwisha? Jibu ni hapana.
Bado kuna safari ndefu, lakini pia kuna nia.
Mafanikio yanaandikwa juu ya mapigano ya jambo hili muhimu.
Kwa hiyo mnaposikia kuhusu rushwa,
msifikiri kwamba hakuna linalotendeka kuhusu hili --
na kwamba hamuwezi kufanya kazi katika nchi yeyote Afrika
kwasababu ya rushwa. Hiyo si kweli.
Kuna nia ya kupambana na rushwa, na katika nchi nyingi, mapambano hayo yanaendelea
na mafanikio yanaonekana. Katika nchi nyingine, kama yangu,
ambako kumekuwa na historia ndefu ya kidikteta nchini Nigeria,
mapambano bado yanaendelea, na bado tuna safari ndefu.
Ukweli wa mambo ni kwamba mapambano bado yanaendelea.
Matokeo yanaonekana:
tathmini huru ya Benki ya Dunia na mashirika mengine
inaonyesha kuwa mwelekeo juu ya rushwa unapungua
na utawala unarekebika.
Utafiti uliofanywa na Tume ya Uchumi ya Afrika unaonyesha
wazi mwelekeo mzuri wa utawala katika nchi 28 za Afrika.
Ngoja niseme kitu kimoja zaidi
kabla sijamaliza kuzungumzia kuhusu utawala bora.
Na ni kitu ambacho watu wanazungumzia kuhusu rushwa, rushwa.
Kila mara wanapo zungumzia kuhusu hili
mara moja unafikiria Afrika.
Hiyo ndio picha: Nchi za Afrika. Lakini ngoja niseme hili:
iwapo Alams alifanikiwa kuhamisha dola za kimarekani milioni 8 kwenye akaunti mjini London --
kama watu wengine waliochukukua pesa wakikadiria kuwa
kati ya bilioni 20 na 40 za pesa za nchi zinazoendelea
ziko nje ya nchi katika nchi zilizoendelea – kama wanaweza kufanyi hivi,
hiyo ni nini? Hiyo siyo rushwa?
Katika nchi hii, kama ukipokea vitu vya wizi, haushitakiwi?
Kwa hiyo tukiongelea kuhusu aina hii ya rushwa, hebu pia tufikirie kuhusu
nini kinatokea katika upande mwingine wa dunia --
ambako pesa hizo zinakwenda na nini kifanyike ili kuweza kuzuia hili.
Kuna jambo ninalifanyia kazi kwa sasa, pamoja na Benki ya Dunia,
kuhusu kurudisha rasilimali, tunajaribu tuwezalo
kurudisha pesa ambazo zimepelekwa nje ya nchi --
pesa za nchi zinazoendelea -- ili ziweze kurudishwa.
Kama tutaweza kurudisha dola bilioni 20 ambazo ziko nje,
litakuwa jambo zuri sana kwa baadhi ya nchi hizi
kuliko misaada yote ikiwekwa pamoja.
(Makofi).
Kitu cha pili ninachotaka kuzungumzia ni nia ya mageuzi.
Afrika, baada – wamechoka, tumechoka
kuwa kitovu cha misaada kutoka kwa kila mtu.
Tunashukuru, ila tunajua kuwa
tunaweza kuchukua hatua juu ya uwezo wetu na kama tuna nia ya kufanya mabadiliko.
Na kinachotokea katika nchi nyingi za Afrika sasa ni utambuzi kwamba
hakuna anayeweza kufanya lolote ila sisi wenyewe. Ni lazima tufanye.
Tunaweza kuwakaribisha washirika ambao wanaweza kutuunga mkono, lakini lazima tuanze wenyewe.
Ni lazima turekebishe uchumi wetu, tubadilishe uongozi,
tuwe na demokrasia zaidi, tuwe wazi kupokea mabadiliko na taarifa.
Na hiki ndicho tumeanza kukifanya
katika mojawapo kati ya nchi kubwa kabisa katika bara, Nigeria.
Hakika, kama hauko Nigeria, hauko Afrika.
Ninataka kuwaambia kuwa.
(Kicheko).
Mmoja kati ya waafrika wanne walio kusini mwa jangwa la Sahara ni Mnigeria,
na ina watu milioni 140 – watu wenye pilika --
lakini watu wenye kuvutia. Hauwezi kuchoka.
(Kicheko).
Tulichoanza kufanya ni kujua kwamba
tunaweza kuchukua hatua na kujibadili wenyewe.
Na kwa msaada wa kiongozi
ambaye alikuwa na nia, kwa wakati ule, ya kufanya mabadiliko,
tunaandaa mpango madhubuti wa mabadiliko
ambao tumeuandika wenyewe.
Si Shirika la Kimataifa la Fedha. Wala Benki ya Dunia,
ambako nilifanya kazi kwa miaka 21 na kufikia cheo cha makamu wa rais.
Hakuna mtu anaweza kukufanyia. Inabidi ufanye mwenyewe.
Tukaandaa mpango ambao kwanza, utafanya: kuiondoa serikali
kwenye shughuli zisizo na manufaa -- zisizoihusu --
Serikali haitakiwi kufanya biashara
ya uzalishaji na utoaji huduma
kwasababu haina ufanisi na haina ujuzi.
Kwa hiyo tuliamua kubinafsisha mashirika yetu mengi.
(Makofi).
Sisi -- matokeo yake, tuliamua kuwa na soko huria.
Unaweza kuamini kuwa kabla ya mabadiliko haya --
ambayo yalianza mwishoni mwa mwaka 2003, wakati nilipoondoka Washington
kwenda kushika nafasi ya Waziri wa Fedha --
tulikuwa na kampuni ya simu ambayo iliweza kutoa huduma za simu za mezani
4,500 katika historia yake ya miaka 30?
(Kicheko).
Kuwa na simu katika nchi yangu lilikuwa ni jambo la kifahari sana.
Usingeweza kupata. Ilibidi uhonge.
Ilibidi ufanye kila uwezalo ili kupata simu.
Rais Obasanjo aliunga mkono na kuzindua
kulegezwa kwa masharti katika sekta ya mawasiliano
tumepanda kutoka simu 4,500 za mezani kufikia simu milioni 32 zenye GSM, na zinaongezeka.
Soko la mawasiliano la Nigeria ni la pili kwa ukuaji duniani kote,♪
ikiwa imetanguliwa na China. Tunapata uwekezaji wa takriban dola bilioni 1 kwa mwaka
katika mawasiliano. Na hakuna mtu anayejua, isipokuwa kwa wajanja wachache.
(Kicheko).
Wajanja wa kwanza kuja
walikuwa ni kampuni ya MTN ya Afrika Kusini.
Katika miaka mitatu niliyokuwa Waziri wa Fedha,
wamepata wastani wa dola milioni 360 kwa mwaka.
milioni 360 katika soko – katika nchi ambayo ni maskini,
yenye wastani wa pato la taifa chini ya dola 500.
Kwahiyo soko lipo hapo.
Walilifanya hili siri, lakini baadae wengine nao walianza kujua.
Wanageria wenyewe walianzisha
makampuni ya mawasiliano ya simu zisizotumia waya
na wengine kama watatu wane hivi wameingia.
Lakini bado kuna soko kubwa sana,
na watu hawajui kuhusu hili, au hawataki kujua.
Kwa hiyo ubinafsishaji ni jambo mojawapo tulilofanya.
Kitu kingine tulichofanya ni kusimamia vizuri masuala yetu ya fedha.
Kwasababu hakuna atakayekusaidia na kukuongoza
iwapo hudhibiti fedha zako vizuri.
Na Nigeria, ikiwa na sekta ya mafuta, ilikuwa na sifa
ya rushwa na kutosimamia vizuri masuala ya fedha za umma.
Je tulijaribu kufanya nini? Tulianzisha sheria ya fedha
ambayo ilitenganisha bajeti yetu na bei ya mafuta.
Zamani tulikuwa tumezoea kubajeti kutokana na kipato ambacho tulikipata kutokana na mafuta,
kwasababu mafuta ndiyo sekta kuu ya mapato
katika uchumi: asilimia 70 ya mapato yetu yanatokana na mafuta.
Tulitenganisha hilo, na tulipofanya hivyo tulianza kubajeti
kwa bei ambayo ilikuwa chini kidogo ya bei ya mafuta
na kuhifadhi chochote cha ziada juu ya bei hiyo.
Hatukuweza kujua kama tungeweza kufanikisha, ilikuwa ni utata sana.®
Lakini kitu ambacho kilitokea haraka ilikuwa ni mabadiliko
ambayo yalikuwepo kwa maendeleo yetu ya uchumi --
ambapo, hata kama bei ya mafuta ingekuwa juu, tungekuwa haraka sana.
Wakati zilipoanguka, tulianguka.
Na tulikuwa tunashindwa kulipia chochote, hata mishahara, katika uchumi.
Hii ilisawazisha. Tuliweza kuweka akiba, kabla sijaondoka,
dola bilioni 27. Ambapo – hii ilienda kwenye hazina yetu --
wakati nilipofika mwaka 2003, tulikuwa na dola billion 7 kwenye akiba.
Na wakati naondoka, tulikuwa na karibu dola bilioni 30. Na
tunavyoongea sasa, tuna dola bilioni 40 kwenye akiba
hii ni kutokana na usimamizi mzuri wa fedha zetu.
Hii inasaidia kutuliza uchumi wetu, kuufanya uwe imara.
Thamani ya fedha yetu ilikuwa ikibadilika kila mara
kwa sasa ipo angalau imara na kusimamiwa, ili wafanyabiashara
wawe na uhakika wa bei katika uchumi.
Tuliweza kudhibiti mfumuko bei kutoka asilimia 28 mpaka karibu asilimia 11.
Na pato letu la taifa liliongezeka kutoka wastani wa asilimia 2.3 kwa muongo uliopita
mpaka kufikia asilimia 6.5 sasa.
Kwa hiyo mabadiliko yote tuliyoweza kufanya
yameweza kuonekana kwa vitendo ambavyo vinaweza kuonekana katika uchumi.
Na kitu cha muhimu zaidi, ni kwasababu tunataka kuondokana na mafuta
na kupanua wigo zaidi – na kuna fursa nyingi sana
katika nchi hii kubwa, kama ilivyo katika nchi nyingine za Afrika --
kilichotia fora zaidi ni huu ukuaji haukutoka
kwenye sekta mafuta pekee, bali sekta nyingine pia.
Kilimo kilikuwa kwa wastani wa asilimi 8.
Sekta ya mawasiliano ilikuwa, makazi na ujenzi,
na ninaweza kuendelea zaidi na zaidi. Na hii ni kuwaonyesha kwamba
uchumi wako unaporekebishika,
fursa katika sekta nyingine zipo nyingi.
Tuna frusa katika kilimo, kama nilivyosema.
Tuna fursa katika madini. Tuna madini mengi
ambako hakuna mtu amewekeza katika utafutaji. Tumegundua
kuwa bila kuwa na sera sahihi za kuwezesha,
hilo halitawezekana. Sasa tuna sheria ya uchimbaji madini
ambayo inalinganishwa na sheria nyingine bora duniani.
Tuna fursa katika makazi na usimamizi wa majumba.
Kulikuwa hakuna chochote katika nchi ya watu milioni 140 --
hakuna maduka makubwa kama myajuavyo hapa.
Hii inaweza kuwa fursa kwa mtu fulani
ambayo ilitia chachu ya kufikiria kwa watu.
Sasa tuna mazingira ambayo biashara katika maduka haya makubwa
yanapata faida mara nne ya ilivyokadiriwa.
Kwa hiyo mambo makubwa kwenye ujenzi, mali isiyohamishika,
Masoko ya rehani. Huduma za fedha
tulikuwa na Benki 89. Nyingi hazifanyi biashara iliyokusudiwa.
Tulizizatiti kutoka 89 kufikia Benki 25 kwa
waongeze mtaji wao -- gawio la mtaji.
Ilikuwa kutoka dola milioni 25 mpaka dola milioni 150.
Benki, Benki hizi sasa zimejizatiti na kuimarishwa
mfumo wa Benki umevutia wamekezaji wengi kutoka nje.
Benki ya Barclays kutoka Uingereza inaingiza milioni 500.
Standard Chartered imeingiza milioni 140.
Ninaweza kuendelea zaidi. Dola zaidi na zaidi, ndani ya mfumo.
Tunafanya hivyo hivyo kwenye sekta ya bima.
Kwa hiyo kwenye huduma za fedha, kuna fursa kubwa zaidi.
Kwenye utalii, katika nchi nyingi za Kiafrika, ni fursa kubwa.
Na hii ndiyo sababu kubwa ya kuwa watu wengi wanaifahamu Afrika Mashariki kwa:
wanyama pori, tembo na kadhalika.
Lakini kusimimamia soko la utalii ili
liweze kuwanufaisha watu ni muhimu sana.
Sasa ninachojaribu kusema ni nini? Najaribu kuwaambia
kuna wimbi jipya katika bara.
Wimbi la uwazi na demokrasia ambapo tangu mwaka 2000,
zaidi ya theluthi mbili ya nchi za Afrika zimefanya
uchaguzi wa kidemokrasia wa vyama vingi.
Si zote zilikuwa kamilifu, au zitakuwa,
lakini mwelekeo uko wazi.
Ninajaribu kuwaelezea kwamba toka miaka mitatu iliyopita
wastani wa ukuaji wa uchumi katika bara umeongezeka
kutoka karibu asilimia 2.5 mpaka asilimia 5 kwa mwaka.
Hii ni bora zaidi ya ufanisi wa nchi nyingi za OECD.
Kwahiyo ni wazi kwamba mambo yanabadilika.
Migogoro imepungua barani;
kutoka migogoro 12 kwa muongo uliopita,
kufikia migogoro mitatu au minne,
Mojawapo ya migogoro mibaya zaidi, kwa hakika, ni ule wa Darfur.
Na kama ujuavyo, kuna athari kwa majirani, iwapo
kuna jambo linatokea upande mmoja wa bara,
inaonekana kama bara zima limeathirika.
Lakini ni vema muelewe kwamba hili bara --
ni bara lenye nchi nyingi na si nchi moja.
Na iwapo tuna migogoro mitatu minne hivi,
ina maana kuwa kuna fursa nyingi za kuwekeza
katika uchumi ulio imara, unaokua na wenye kusisimua
ambako kuna fursa nyingi sana.
Ningependa kutoa dokezo moja kuhusu uwekezaji huu.
Namna nzuri ya kuisaidia Afrika sasa
ni kuwasaidia waweze kusimama wenyewe.
Na namna nzuri ya kufanya hivyo ni kusaidia kuleta ajira.
Hakuna tatizo katika kupambana na malaria na kuwekeza pesa kwenye hilo
na kuokoa maisha ya watoto. Sina maana hiyo. Hilo ni sawa.
Lakini fikiria tofauti itakayokuwa kwenye familia: iwapo wazazi wanaweza kuwa na ajira
na wakahakikisha watoto wao wanakwenda shule,
kwamba wanaweza kununua dawa za kupambana na magonjwa wao wenyewe.
Kama tunaweza kuwekeza kwenye maeneo ambayo nyinyi wenyewe mnapata faida
wakati huo huo mkitengeneza ajira na kuwasaidia watu wasimame wenyewe,
hii siyo fursa nzuri? Hii si ndiyo njia ya kufuata?
Na nataka kusema jambo kuhusu watu bora zaidi wa kuwawekezea
katika bara hili ni wanawake.
(Makofi).
Nina CD hapa. Samahani sikusema kwa wakati muafaka.
Lakini, ningependa mngekuwa mmeiangalia.
Inasema, "Afrika: Iko wazi kwa Biashara."
Na video hii imeshinda tuzo
kama makala bora ya mwaka.
Elewa kwamba mwanamke aliyetengeneza makala hii
atakuwa Tanzania, ambako watakuwa na kongamano mwezi Juni.
Lakini hii inakuonyesha kwamba Waafrika, na hususani wanawake wa Afrika, ambao
pamoja na matatizo yote wameweza kuanzisha biashara, nyingine ni za kiwango cha kimataifa.
Mmoja kati ya wanawake katika video hii, Adenike Ogunlesi,
anashona nguo za watoto
kitu ambacho alianza kama kujifurahisha na ikakua na kuwa biashara.
Akichanganya vitambaa vya Kiafrika ambavyo tunavyo,
na vitambaa vingine kutoka sehemu nyingine.
Na hivyo, atatengeneza suruali kwa kutumia vitambaa vizito,
ikiwa imechanganywa na vitambaa vya kiafrika. Ni ubunifu mzuri sana.
Amefikai hatua ambapo anapata zabuni kutoka Wal-Mart.
(Kicheko).
Kwa nguo 10,000
Kwa hiyo hii inawaonyesha kuwa tuna watu wenye uwezo wa kufanya mambo.
Wanawake wana juhudi, wako makini; wanachapa kazi.
Naweza kuendelea kwa kutoa mifano:
Beatrice Gakuba wa Rwanda, alifungua biashara ya maua
na sasa anayasafirisha kwenye mnada wa udachi huko Amsterdam kila asubuhi,
na ameajiri wanawake na wanaume takriban 200 kumsaidia kazi.
Hata hivyo, wengi wao, wana kiu ya kupata mtaji wa kupanua biashara zao,
kwasababu hakuna anayeamini nje ya nchi zetu
tunaweza kufanya mambo ya maana. Hakuna mtu anayefikiria kwa mtazamo wa masoko.
Hakuna anyefikiria kuna fursa
Nimesimama hapa kuwaambia wale waliochelewa jahazi kwa sasa,
watalikosa milele.
Kwa hiyo iwapo unataka kuwa Afrika, fikiria kuwekeza.
Wafikirie akina Beatrice, wafikirie kina Adenike wa dunia hii.
ambao wanafanya mambo makubwa ambayo yanawasogeza
katika uchumi wa dunia, wakati huo huo wakihakikisha
wanawake wenzao na wanaume wanapata ajira.
na kwamba watoto katika familia hizo wanapata elimu
kwa sababu wazazi wao wanapata kipato cha kuridhisha
Kwa hiyo nina wakaribisha kuja kutafuta fursa
Mtakapo kwenda Tanzania, sikilizeni kwa makini,
kwasababu nina hakika mtasikia kuhusu fursa mbalimbali zilizopo
ili muweze kushiriki katika kufanya mambo mazuri
kwa bara hili, kwa watu wake na kwenu wenyewe
Asanteni sana.
(Makofi)