Nataka niwaambie kisa kuhusu msichana mmoja. Lakini siwezi kuwaambia jina lake halisi. Hivyo tufanye kumuita Hadiza. Hadiza ana miaka 20. Ana aibu, lakini ana tabasamu zuri ambalo hufanya uso wake kung'aa Lakini yuko katika maumivu wakati wote. Na anaweza kuwa mtu wa matibabu maisha yake yote. Je wataka kujua kwa nini? Hadiza ni msichana wa Chibok, na mnamo Aprili 14, 2014, alitekwa na magaidi wa Boko Haram. Ingawa alijaribu kutoroka, kwa kuruka toka kwenye gari lililokuwa limebeba wasichana. Lakini alipotua chini, alivunjika miguu yako yote miwili, na alihitaji kutambaa kwa tumbo kujificha kichakani. Aliniambia aliogopa sana kuwa Boko Haram wangeweza kumrudia. Alikuwa mmoja wa wasichana 57 waliotoroka kwa kuruka toka kwenye magari siku ile. Kisa hiki, hakika, kilisambaa kama mawimbi duniani kote. Watu kama Michelle Obama, Malala na wengine walitoa sauti zao wakipinga, na wakati huo huo -- nilikuwa nikiishi London wati huo Nilitumwa kutoka London kwenda Abuja kupata habari za Jukwaa la Uchumi Duniani ambapo Naijeria ilikuwa mwenyeji kwa mara ya kwanza Lakini nilipofika, ilikuwa dhahiri kwamba kulikuwa na habari moja tu mjini. Tuliiiweka serikali kwenye shinikizo. Tuliuliza maswali magumu juu ya nini wanafanya kuwarudisha wasichana hawa. Ilieleweka hakika, hawakuwa na furaha juu ya maswali yetu, na tuseme tu tulipata mgao mzuri wa "ukweli mbadala". (Kicheko) Wanaijeria wenye ushawishi mkubwa walikuwa wakituambia wakati ule kuwa tulikuwa washamba. hatukuelewa hali ya siasa ya Naijeria. Lakini pia walituambia kuwa habari ya wasichana wa Chibok illikuwa mzaha. Cha kusikitisha ni kuwa habari hii ya mzaha imedumu na bado kuna watu Naijeria leo wanaoamini wasichana wa Chibok hawakutekwa. Bado, nilikuwa nikiongea na watu kama hawa wazazi wenye huzuni kubwa, ambao walituambia siku Boko Haram waliwateka binti zao, walikimbia mpaka Msitu wa Sambisa wakifukuza magari laliyobeba binti zao. Wao walikuwa na mapanga kama silaha, lakini walilazimika kurudi sababu Boko Haram walikuwa na bunduki. Kwa miaka miwili, pasipo kuepukika, ajenda za habari zilisonga mbele, na kwa miaka miwili, hatukusikia sana kuhusu wasichana wa Chibok. Kila moja alidhania wamekwishakufa. Lakini Aprili mwaka jana, niliweza kupata video hii. Hii ni picha-mnato toka kwenye video ambayo Boko Haram walirekodi kama ushahidi kuwa wako hai, na kupitia chanzo kimoja, nilipata video hii. Lakini kabla sijaichapisha, Nilihitaji kusafiri kwenda kaskazini mashariki mwa Naijeria kuzungumza na wazazi, kuihakikisha. Sikuhitaji kusubiri sana kupata uthibitisho. Mmoja wa wamama, alipoangalia hiyo video, aliniambia kama angeweza kuifika ndani ya kompyuta na kumvuta na kumtoa nje mtoto wake kutoka kwenye kompyuta, angefanya hivyo. Kwa wale kati yenu ambao ni wazazi, kama mimi, katika wasikilizaji. Mnaweza tu kufikiria uchungu ambao yule mama aliusikia Video hii iliendelea hadi kuanzisha mjadala wa mazungumzo na Boko Haram. Na seneta mmoja wa Kinaijeria aliniambia kuwa kwa sababu ya video hii waliingia katika yale mazungumzo, kwa sababu muda mrefu walidhani wasichana wa Chibok walishakufa. Wasichana 21 waliachiwa huru mwezi Oktoba mwaka jana. Cha kusikitisha, karibu 200 kati yao bado hawajapatikana. Ni lazima nikiri, sijawa mwangalizi niliyependelea kuzungumzia habari hii. Nakuwa na hasira ninapofikiria juu ya fursa zinazopotea kuwaokoa wasichana hawa. Nakuwa na hasira ninapofikiria juu ya kile wazazi wameniambia, kuwa ingekuwa mabinti hawa ni wa matajiri na wenye nguvu, wangepatikana mapema zaidi. Na nina hasira kwamba simulizi la mzaha ambalo naamini hakika limesababisha kuchelewa; lilikuwa ni sehemu ya sababu ya ucheleweshwaji wa kurudi kwao. Hii inaonesha kwangu hatari kubwa ya habari za uongo. Nini twaweza kufanya juu ya hili? Kuna watu werevu sana, wahandisi werevu huko Google na Facebook, wanaojaribu kutumia tekinolojia kuzuia kusambaa kwa habari za uongo. Lakini zaidi ya hapo, nafikiri kila mmoja hapa -- wewe na mimi -- tuna nafasi ya kushiriki katika hilo. Sisi ndio tunaoshirikishana maudhui Sisi ndio tunaoshirikishana habari mitandaoni Nyakati za leo, sisi sote ni wachapishaji, na tuna jukumu. Katika kazi yangu kama mwanahabari, Ninaangalia, ninathibitisha, Ninaamini hisia zangu, lakini nauliza maswali magumu. Kwa nini huyu mtu ananiambia habari hii? Nini atakachokipata kwa kunishirikisha taarifa hii? Je, ana ajenda ya siri? Ninaamini kabisa kuwa wote tunatakiwa kuanza kuuliza maswali magumu zaidi kwa taarifa tunazozipata mtandaoni. Utafiti unaonesha kwamba kati yetu kuna wasiosoma zaidi ya vichwa vya habari kabla ya kushirikisha habari. Nani hapa amefanya hivyo? Najua mimi nimefanya. Lakini ingekuwaje kama tungeacha kuchukua taarifa tuipatayo jinsi ionekanavyo kijuujuu? vipi kama tutasimama na kufikiria athari za taarifa ambazo tunazisambaza na uwezo wake wa kuchochea vurugu na chuki? Vipi kama tutasimama na kufikiria juu ya athari kwenye maisha halisi za taarifa tunazoshirikishana? Ahsanteni sana kwa kunisikiliza. (Makofi na vifijo)