Nilikuwa na umri wa miaka 14 nikiwa kwenye jumba la michezo, nikiiba kwenye mashine ya mchezo, na nilipokuwa nikitoka nje ya jengo mlinzi alikamata mkono wangu, hivyo nikakimbia. Nilikimbilia mtaani, na nikaruka juu ya uzio. Na nilipofika juu, uzito wa sarafu 3,000 kwenye mkoba wangu ulinielemea na kunivuta chini. Niliponyanyuka, mlinzi alikuwa amesima juu yangu, na akasema, "Siku nyingine nyinyi vibaka, ibeni vitu mnavyoweza kubeba." (Kicheko) Nilipelekwa kwenye mahabusu ya watoto na nilipoachiliwa chini ya dhamana ya mama yangu, maneno ya kwanza mjomba wangu alisema yalikuwa, "Ulikamatwaje?" Nikasema, "Mzee, mkoba ulikuwa mzito sana." Akasema, "Mzee, hukutakiwa kuchukua sarafu zote." Nikasema, "Mzee, zilikuwa ndogo. Ningefanyaje?" na dakika 10 baadaye, alinipeleka kuiba kwenye mashine nyingine ya mchezo. Tulihitaji pesa ya petroli kufika maskani. Hayo ndiyo yalikuwa maisha yangu. Nimekulia Oakland, Kalifornia, na mama yangu na ndugu wa karibu wa familia walevi wa madawa ya kulevya ya kokeini . Mazingira yangu yalijumuisha kuishi na familia, marafiki, na makazi kwa wasio-na-makazi. Mara nyingi, mlo wa jioni tuliupata kwenye foleni za vyakula vya msaada. Mjomba aliniambia hivi: pesa inatawala dunia na kila kitu ndani yake. Na katika hii mitaa, pesa ni Mfalme. Na ikiwa utafuata pesa, itakupeleka kwa mtu mbaya au mtu mzuri. Baadaye kidogo, nilifanya uhalifu wangu wa kwanza, na ndiyo mara ya kwanza nilipoambiwa kuwa nina kipaji na nikajisikia kuwa kuna mtu ananiaminia. Hakuna aliyewahi-niambia kuwa ningeweza kuwa mwanasheria, daktari au mhandisi. Yaani, ningewezaje kufanya hivyo? Sikuweza kusoma, kuandika wala kutahajia. Sikuwa mtu aliyesoma. Kwahiyo, mara zote nilifikiri uhalifu ndio njia ya kwenda. Na kisha siku moja Nilikuwa naongea na mtu na alikuwa ananiambia juu ya huu wizi ambao tungeweza fanya. Na tukaufanya. Ukweli ni kwamba nilikuwa nakulia kwenye nchi yenye uwezo mkubwa wa kifedha duniani, Marekani, huku nikiangalia mama yangu, akisimama kwenye foleni ya benki ya damu kuuza damu yake kwa Dola 40 kujaribu tu kulisha wanae. Bado ana alama za sindano mikononi mwake leo kudhihirisha hilo. Kwa hiyo sikuijali jumuiya yangu, Hawakujali maisha yangu. Kila mtu pale alifanya anachotaka fanya kupata alichotaka, wauza mihadarati, wezi, benki ya damu. Kila mtu alichukua fedha ya damu. Hivyo nilipata yangu kwa njia yoyote ile. Nilipata yangu. Elimu ya fedha kweli ilitawala dunia, na nilikuwa mtoto mtumwa kwake nikifuata mtu mbaya. Nikiwa na miaka 17, nilikamatwa kwa wizi na mauaji na punde nikajifunza kuwa fedha jela zinatawala zaidi ya zilivyo mitaani, Hivyo nilitaka kuingia. Siku moja, nilikurupuka kushika ukurasa wa michezo katika gazeti ili mfungwa mwenzangu anisomee, na kwa bahati mbaya nikachukua sehemu ya biashara. Na huyu mzee akasema, "Hey, kijana, umechukua hisa?" Na nikasema, "Ndio nini hicho?" Akasema, "Hiyo ndiyo sehemu ambayo watu weupe huweka pesa yao yote." (Kicheko) Na ilikuwa ndiyo mara ya kwanza nilipata ono fupi la tumaini, siku za baadaye. Alinipa maelezo mafupi ya hisa zilikuwa ni nini, lakini ilikuwa ni muhtasari tu. Yaani, ningewezaje kuifanya? Sikuweza kusoma, kuandika wala kutahajia. Ujuzi niliokuwa nimeukuza kuficha kutokusoma kwangu haukufanya kazi tena katika mazingira haya. Nilikuwa nimenaswa kwenye kizimba mateka kati ya watekaji, nikipigania uhuru ambao sijawahi kuwa nao. Nilikuwa nimepotea, nimechoka, na sikuwa na machaguzi. Kwa hiyo nikiwa na miaka 20, nilifanya kitu kigumu kuliko vyote nilivyowahi kufanya maishani mwangu. Nilichukua kitabu, na ilikuwa ni kipindi kigumu sana maishani mwangu. kujaribu kujifunza jinsi ya kusoma, kutengana na familia yangu, na rafiki zangu. Ilikuwa shida, mzee. Ilikuwa ni mahangaiko. Lakini sikufahamu japo kidogo kuwa nilikuwa napata zawadi kubwa kuliko zote nilizowahi kuziota, kujithamini, maarifa, nidhamu. Nilisisimka mno kusoma, kiasi kwamba nilisoma kila kitu nilichokitia mkononi: makaratasi ya pipi, nembo za nguo, alama za barabarani, kila kitu. Nilikuwa nikisoma tu vitu! (Makofi na Vifijo) kusoma tu vitu. Nilisisimka sana kujua jinsi ya kusoma na kujua jinsi ya kutahajia. Rafiki alikuja, akaniuliza, "Mzee, unakula nini?" Nikasema, "P-I-P-I, pipi." (Kicheko) Akasema, "Nipe kidogo." Nikasema, "L-A. La." (Kicheko) Ilikuwa babukubwa. Yaani, sasa naweza, kwa mara ya kwanza katika maisha yangu, kusoma. Hisia niliyoipata, ni ya kustaajabu sana. Kisha, nikiwa na miaka 22, nikijisikia mwenyewe, nikijiamini, Nilikumbuka kile yule mzee aliniambia. Kwa hiyo nilichukua kurasa za biashara za gazeti. Nilitaka kuwatafuta hawa matajiri weupe. (Kicheko) Kwa hiyo nilitafuta ule muhtasari. Nilipokuwa nikijiendeleza kikazi nikifundisha wengine namna ya kusimamia fedha na kuwekeza, punde nikajifunza kuwa nilihitaji kuwajibika kwa matendo yangu. Kweli, nilikulia kwenye mazingira tata sana, lakini nilichagua kufanya uhalifu, na nilipaswa kukiri hilo. Nilipaswa kuwajibika kwa hilo, na nilifanya hivyo. Nilikuwa nikiunda mtaala ambao ungeweza kuwafundisha wafungwa namna ya kusimamia fedha kupitia ajira za gerezani. Kutiisha mtindo wetu wa maisha kungeweza kutoa zana zihamishikazo ambazo tunaweza kuzitumia kusimamia fedha tunapoirudi kwenye jamii, kama watu wengi walivyofanya ambao hawakufanya uhalifu. Kisha niligundua kulingana takwimu ya MarketWatch, zaidi ya asilimia 60 ya wakazi wa Marekani wana chini ya Dola 1,000 katika akiba. Michezo ilielezea kwamba zaidi ya asilimia 60 ya wachezaji wa NBA na wachezaji wa NFL hufilisika. Asilimia 40 ya matatizo ya ndoa hutokana na masuala ya kifedha. Balaa gani? (Kicheko) Unataka kuniambia, watu wamefanya kazi maisha yao yote, wakinunua magari, nguo, nyumba na vitu mbalimbali lakini walikuwa waliishi hundi kwa hundi? Ni namna gani duniani wanajamii wangekwenda kuwasaidia wafungwa kurudi kwenye jamii ikiwa hawakuweza kusimamia mambo yao wenyewe? Tumevurugwa. (Kicheko) Nahitaji mpango mzuri zaidi. Hii haitakwenda kufanya kazi vizuri. Hivyo ... Nilifikiria. Sasa nilikuwa na wajibu kukutana na wale waliokuwa kwenye mkondo huo na kuwasaidia, na ilikuwa ni ajabu sababu sasa nilijali jumuiya yangu Lo, hebu fikiria. Nilijali kuhusu jumuiya yangu. Ujinga juu ya Fedha ni ugonjwa ambao umedhohofisha wachache na walio chini katika jamii yetu kwa vizazi na vizazi, na tunapaswa kukasirika juu ya hilo. Ebu jiulize: Inawezekanaje asilimia 50 ya wakazi wa Marekani wasiwe na elimu ya fedha katika nchi inayoendeshwa kwa ustawi wa kifedha? Kupatikana kwa haki kwetu, hadhi yetu ya kijamii, hali ya maisha, usafirishaji na chakula vyote vinategemea fedha ambayo watu wengi hawawezi kuisimamia. Ni ajabu! Ni janga na hatari kubwa kwa usalama wa umma kuliko suala jingine lolote. Kadiri ya Kitengo cha Urekebishaji cha Kalifornia, zaidi ya asilimia 70 ya wale waliofungwa wamefanya au wameshtakiwa kwa uhalifu uhusianao na fedha: wizi wa kutumia nguvu, kuvunja nyumba, kutapeli, uporaji, ghusubu -- na orodha inaendelea. Angalia hii: Mfungwa wa kawaida huingia katika mfumo wa gereza wa Kalifornia pasipo kuwa na elimu ya fedha, hupata ujira wa senti 30 kwa saa, zaidi ya Dola 800 kwa mwaka, bila ya kuwa na matumizi yoyote na kuweka akiba yoyote. Anapopewa msamaha, hupewa dola 200 pesa ya geti na kuambiwa, "Wee, mafanikio mema, kaa mbali na matatizo. Usirudi gerezani tena." Bila kuwa na maandalizi yoyote ya maana au mpango fedha wa muda mrefu, anafanyaje ...? Akiwa na miaka 60? Apate kazi nzuri, au arudi kwenye tabia ile ile ya uhalifu iliyompeleka gerezani kwanza? Nyinyi walipakodi, chagueni wenyewe. Hakika, elimu yake imeshamchagulia, pengine. Kwa hiyo, tunatibuje ugonjwa huu? Nilishiriki kuanzisha programu tuliyoiita Elimu Hisia ya Uwezeshaji wa Kifedha tunaiita FEEL na inafundisha namna ya kutenganisha maamuzi ya kihisia na maamuzi ya kifedha, na sheria 4 aushi za utawala fedha binafsi: njia sahihi ya kuweka akiba, kudhibiti gharama zako za maisha, kukopa fedha kwenye ufanisi kutawanya fedha yako kuruhusu fedha yako ikufanyie kazi badala ya wewe kuifanyia kazi. Wafungwa wanahitaji ujuzi huu kabla ya kuingia tena kwenye jamii. Hatuwezi kubadilika kuwa na maisha ya kawaida bila ujuzi huu wa maisha. Hii dhana kuwa ni Weledi tu wanaweza kuwekeza na kusimamia fedha ni ya fedheha kabisa, na yeyote aliyewaambia hivyo anadanganya. (Makofi na Vifijo) Mweledi ni mtu anayejua kazi zake kuliko walio wengi, na hakuna mtu ajuaye kiasi gani cha fedha wahitaji, unacho, au wataka zaidi ya wewe, ikimaanisha kuwa wewe ni mweledi. Elimu ya fedha siyo stadi, mabibi na mabwana. Ni mtindo wa maisha. Uimara wa kifedha ni matokeo ya ziada ya mtindo sahihi wa maisha. Mfungwa mwenye elimu nzuri ya kifedha anaweza kuwa mwananchi mlipakodi, na mwananchi mlipakodi mwenye elimu nzuri ya kifedha anaweza kubaki hivyo. Hii inatuwezesha kuunda daraja kati ya wale watu tunaowashawishi: familia, marafiki na wale vijana ambao bado wanaamini kuwa uhalifu na pesa vina uhusiano. Kwa hiyo tupoteze uwoga na wasiwasi wa maneno makubwa ya kifedha na ujinga mwingine wote ambao mmekuwa mkisikia huko nje. Na tujikite kwenye kiini kilichokuwa kinadhoofisha jamii yetu kuanzia kutimiza wajibu wako la kuwa meneja mzuri wa maisha. Na tutoe mtaala mwepesi na rahisi kutumia ambao utaingia kwenye kiini, kiini cha ni nini ukweli wa uwezeshaji wa kifedha na elimu ya hisia. Sasa, ikiwa umekaa hapa kwa wasikilizaji na umesema, "Ndiyo, kweli, hiyo si mimi na sikubaliani nayo," basi njoo uchukue somo langu -- (Kicheko) ili nikuoneshe ni kiasi gani cha pesa inakugharimu kila unaposhikwa na hisia. (Makofi na Vifijo) Asanteni sana. Asanteni. (Makofi na Vifijo)